KISWAHILI Form 2 Topic 3

UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI SIMULIZI
Fasihi simulizi kama zilivyo kazi nyingine za fasihi andishi hufanyiwa uhakiki. Uhakiki huu huzingatia vipengele vya fani na maudhui ili kubainisha usanaa wa kazi husika pamoja na kile ilichokusudia kufikishwa kwa hadhira.
Mashairi kama kazi nyingine za kifasihi huhakikiwa kwa kutumia vigezo sawa na vinavyotumika katika kazi nyingine za kifasihi. Vigezo hivyo ni kwa kuzingatia vipengele vyake viwili yaani fani na maudhui.
Vipengele vya Fani na Maudhui katika Kuhakiki Ushairi
Elezea vipengele vya fani na maudhui katika kuhakiki ushairi
Vipengele vya fani
Uhakiki wa fani za ushairi ni uchambuzi wa kina na kuziweka wazi mbinu za kisanaa alizotumia mshairi katika kutunga kazi yake. Vipengele muhimu vya kuhakiki katika fani ya ushairi ni kama vifuatavyo:
Mtindo
Jambo la kuonyesha hapa ni kwamba iwapo shairi ni la kimapokeo ama ni la kisasa.
Muundo
Katika kuhakiki muundo wa shairi mhakiki inatakiwa aweke wazi mambo yafutayo:
 1. Idadi ya beti
 2. Idadi ya mistari na aina ya vibwagizo
 3. Idadi ya vipande
 4. Idadi ya mizani
 5. Aina na mpangilio wa vina
Wahusika
Ikiwa shairi limehusisha wahusika ni vema pia mhakiki awabainishe
Matumizi ya lugha
Katika kipengele hiki mhakiki huchunguza:
 1. Mpangilio wa maneno. Mf. Wengi wari badala ya wari wengi
 2. Matumizi ya : Mazida – kurefusha neno mfano, kiwembe badala ya wembe; Ikisari – kufupisha neno mfano siombe badala ya usiombe; Tabdila – kubadilisha mwendelezo wa neno mfano kujitanuwa badala ya kujitanua.
 3. Matumizi ya methali, misemo na nahau
 4. Matumizi ya lugha ya picha
 5. Matumizi ya tamathali za semi kama vile takriri, sitiari n.k
 6. Mbinu nyingine za kisanaa
Mhakiki anapochunguza vipengele vya fani, jambo muhimu la kuzingatia ni jinsi vipengele hivyo vinavyosaidia kuwasilisha maudhui.
Vipengele vya maudhui
Ili kuhakiki na kupata maudhui ya shairi inatakiwa kulisoma shairi kwa kulielewa zaidi. Baada ya kupata picha fulani kuhusu shairi na kutafakari maana za maneno muhimu, itatubidi tuelewe vipengele vya maudhui, ambavyo ni dhamira, mtazamo, msimamo, falsafa ya mwandishi, ujumbe na maadili, migogoro na muktadha.


Igizo huhakikiwa kwa namna lilivyo katika maumbo yake yote mawili yaani fani na maudhui.
Vipengele vya Fani na Maudhui katika Kuhakiki Maigizo
Elezea vipengele vya fani na maudhui katika kuhakiki maigizo
Fani
Uhakiki wa fani katika maigizo unajihusisha na ufundi uliotumiwa. Ufundi huu unajumuisha mambo kadhaa kama ifuatavyo:
Mtindo
Mtindo ni sura ya maigizo inayojitokeza kupitia mpangilio wa maneno na vitendo. Inabidi mhakiki achunguze kama kazi ni:
 1. Mchezo wa jukwaani – wenye mpangilio wa mazungumzo baina ya watu na matendo yao.
 2. Majigambo
 3. Vichekesho – mpangilio wa maneno yanayowasilisha ujumbe kwa kuchekesha.
 4. Mazungumzo – maongezi ya kujibizana baina ya watu.
 5. Ngonjera – mpangilio wa tungo za kishairi ambapo watu wawili au makundi mawili hukinzana.
 6. Miviga – sherehe za kitamaduni kama vile matambiko
Pamoja na haya, mtindo hutegemea lengo la maigizo ambalo laweza kuwa kuelimisha, kukejeli, kuburudisha, kuonya, kukosoa na kadhalika.
Mandhari
Mazingira ya kutendea ni kipengele muhimu cha fani. Mhakiki hana budi kujiuliza iwapo utendaji unadhihirisha wakati au mahali halisi. Jambo hili huweza kutekelezwa kupitia vifaa, maleba, maneno n.k.
Wahusika
Maswali ya mhakiki kuuliza ni:
 • Wamejitokeza kikamilifu?
 • Wanaaminika?
Matumizi ya lugha
Vigezo anavyotumia mhakiki kuchunguza lugha ni:
 • Kama usemaji ni wa kisanaa, yaani unatumia picha, tamathali za semi, methali, nahau n.k.
 • Kama lugha imetumika vile inavyotumiwa katika jamii. Mfano: kiimbo, mkazo, miguno, vihisishi n.k.
 • Matumizi ya maneno ya ajabu kama yale yanayotumiwa na waganga.
Maleba na vifaa
Hivi huakisi mandhari na husaidia kuzua mukatadha. Kwa hiyo ni muhimu kuchunguza kama vimetumiwa ipasavyo.
Matumizi ya ala
Matumizi ya ala kama ngoma, baragumu, au sauti zingine ili kuamsha hisia za hadhira ni jambo muhimu kuchunguza.
Mbinu nyingine
Mhakiki anapaswa pia kuchunguza matumizi ya nyimbo, uchezaji ngoma, usimulizi na mbinu nyingine katika kuibua hisia za watazamaji.
Maudhui
Kwa upande wa maudhui, mhakiki wa maudhui hutakiwa kuchunguza vipengele vyote vya kimaudhui ambavyo ni dhamira, migogoro, maadili, mtazamo na msimamo wa fanani pamoja na ujumbe bila kusahau kipengele cha falsafa. Yote hayo kwa pamoja ndiyo humsaidia mhakiki kubaini ukinzani wa igizo na maisha halisi ya jamii ambayo huwa ndiyo hadhira ya igizo hilo.